Friday, October 14, 2016

KISUKARI ( DIABETES MELLITUS )

Kisukari ni miongoni mwa matatizo ya kiafya yanayowapata watu wengi .Tatizo hili linatokana na kuwepo kwa kiwango kikubwa cha sukari kwenye damu (Blood sugar) kuliko mahitaji ya mwili kwa wakati huo kutokana na kushindwa kwa mfumo wa urekebishaji kiwango cha sukari kwenye damu. Baadhi ya viungo vinavyohusika na urekebishaji sukari ni kama vile Kongosho (pancrease) na ini. Kuongezeka kwa sukari kwenye damu kunaweza sababishwa na aidha kongosho kushindwa kuzalisha homoni ya insulin inayosaidia kushusha kiwango cha sukari  (Type I Diabetes mellitus) au Tishu ya mwili kushindwa kuchukua insulinin ili kushusha sukari (Type II Diabetes mellitus).


                  AINA ZA KISUKARI

Kongosho
1.TYPE I DIABETES MELLITUS
  Aina hii ya kisukari hutokana na kongosho kushindwa kuzalisha hormone ya insulin kutokana na kuharibiwa kwa beta cells zinazozalisha hormone hii na kufanya mwili kushindwa kushusha kiwango cha sukari kwenye damu.


2.TYPE II DIABETES MELLITUS 
Aina hii ya kisukari  hutokea kutokana kushindwa kwa tishu za mwili kuchukua hormone ya insulin ili kushusha kiwango cha sukari (Tissue resistance). Hali hupelekea kongosho kuzalisha insulin kuliko uwezo wake ambapo mwishoni kongosho hushindwa kuzalisha insulin kabisa..
       Kuna sababu  mbalimbali zinazosababisha tatizo la kisukari kama inavyooneshwa hapa chini

SABABU ZINAZOWEZA KUPELEKEA KUPATA KISUKARI

                              1.Kuwa na uzito mkubwa kupita kiasi














   2.Sababu za  urithi. Tafiti zinaonesha kuwepo kwa genes ambazo hupelekea kongosho kushindwa kuzalisha insulin kwa watu wenye kisukari ambapo huweza kurithiwa kutoka kizazi kimoja kwenda kizazi kingine.

                   3.Magonjwa ya kongosho kama Pancreatitis

                                                        4.Kutumia kilevi.






                         DALILI ZA KISUKARI



  1. Kuhisi kiu ya maji mara kwa mara
  2. Kunywa maji mengi
  3. Kukojoa mkojo wenye sukari
  4. Kusikia njaa mara kwa mara
  5. Macho kushindwa kuona 
  6. Vidonda visivyopona haraka
  7. Kuwa na uchovu 







        NJIA ZA KUEPUKANA NA KISUKARI



 


  1.  Hakikisha uzito wa mwili wako hauwi mkubwa kwa kufanya mazoezi
  2. Epuka kula chakula kinachoongeza mafuta kupita kiasi
  3. Jenga mazoea ya kupunguza matumizi ya kilevi
  4. Nenda hospitali mara kwa mara kujua hali ya afya yako.



LINKS:
http://www.webmd.com/diabetes/guide/types-of-diabetes-mellitus

https://www.betterhealth.vic.gov.au/health/tentips/10-tips-to-help-prevent-type-2-diabetes

Preapared by Andrew Luhusa ,MD Student @MUHAS
              
                               14TH OCT 2016.

Thursday, October 6, 2016

VIDONDA VYA TUMBO (PEPTIC ULCER DISEASE)



Vidonda vya tumbo ni tatizo linalotokea kwenye mfumo wa chakula ambapo kuta za tumbo au utumbo hushambuliwa na bacteria waitwao
  helicobacter pylori na kusababisha kuwepo kwa vidonda kwenye kuta za tumbo au utumbo na kuambatana na maumivu makali. Bacteria hawa huweza kukaa kwa muda mrefu ndani ya tumbo bila kuleta madhara hadi pale pindi watakapochochewa kuanza kushambulia kutokana na sababu mbalimbali za kimazingira ,kama utumiaji wa pombe na madawa kama aspirin kwa muda mrefu.
Helicobacter pylori
















SABABU HATARISHI ZINAZOWEZA KUPELEKEA KUPATA VIDONDA VYA TUMBO

1.Matumizi ya dawa aina ya aspirin (Non steroidal anti inflammatory drugs{NSAIDs}) kwa muda mrefu hupelekea kusababisha tatizo la vidonda vya tumbo. Dawa hizi huzuia kutengenezwa kwa kemikali iitwayo prostaglandin ambayo husaidia katika kuimarisha kuta za utumbo . Hivyo kushinndwa kuimarika kwa kuta za tumbo hufanya kuwepo urahisi wa kushambuiliwa na bacteria na kusababisha vidonda.






2.Matumizi ya pombe kupita kiasi husababisha kupungua kwa uwezo wa ndani wa kuta za tumbo (Epithelial lining) kuzuia tindikali ya tumbon kutokuharibu ukuta wa ndani wa tumbo( Mucosal barrier).Hali hii hufanya tindikali pamoja na bacteria kupenya kwa urahisi kuingia kwenye kuta za tumbo na kusababisha vidonda.


stress


3. Uvutaji sigara pia waeza kupelekea kupata tatizo la vidonda vya tumbo.

4.Msongo wa mawazo



DALILI ZA VIDONDA VYA TUMBO

1.Maumivu ya tumbo

2. Kiungulia

3.Kupungua uzito

4.Kichefuchefu na kutapika

5.Tumbo kujaa gas

NAMNA YA KUEPUKANA NA VIDONDA VYA TUMBO

1.Epuka matumizi ya kilevi kupita kiasi


2.Epuka matumizi ya sigara

3.Tumia dawa pale unaposhauriwa na daktari.na epuka matumizi ya aspirin (NSAIDs)

4.Kula chakula bora na mlo kamili usiokuwa na tindikali nyingi.

5.Punguza msongo wa mawazo





LINKS;

1.http://www.webmd.com/digestive-disorders/tc/peptic-ulcer-disease-what-increases-your-risk

2.http://www.healthline.com/health/stomachulcer

3.http://www.mayoclinic.org/diseases-conditions/peptic-ulcer/manage/ptc-20231410

Prepared by Andrew Luhusa; MD student @ MUHAS
                            
                                     7th Oct 2016

Friday, September 30, 2016

SHINIKIZO LA DAMU (HYPERTENSION)

SHINIKIZO LA DAMU (HYPERTENSION)

Shinikizo kubwa la damu ni tatizo linalotokea katika mfumo wa mzunguko wa damu ambapo kiwango cha pressure ya damu huzidi kiwango cha kawaida ambacho huwa ni 120/80mmHg kwa mtu mzima mwenye afya nzuri.Shinikizo la damu kuwa kubwa kupita kiasi ni hatari kwa afya zetu. Tatizo huanza kuwa kubwa pale pressure ya damu inapofikia 140/90mmHg.Shinikizo kubwa la damu laweza kugawanywa katika makundi mawili kutokana na sababu za tatizo hilo, kuwa ni sababu kadhaa za kimazingira au kurithi (Esential /primary hypertension) ama kutokana na tatizo fulani kwenye mwili kwa mfano Figo kushindwa kufanya kazi (Secondary hypetension).



SABABU ZINAZOWEZA KUPELEKEA KUPATA TATIZO LA SHINIKIZO KUBWA LA DAMU

1.Kuwa na uzito mkubwa kupita kiasi (Obesity).Uzito mkubwa kupita kiasi unatokana na kuwepo mafuta mengi mwilini kuliko yanayotakiwa mwilini.Hali hii hupelekea kurundikana kwa mafuta kwenye Organ
mbalimbali kama moyo,ini na mishipa ya damu(arteries).Hupunguza kipenyo cha mishipa ya damu na kupelekea shinikizo kubwa la damu.

2..Msongo wa mawazo (stress). kuwa  na msongo wa mawazo huathiri mfumo wa mzunguko wa damu na kufanya moyo kusukuma damu kwa nguvu, hali inayopelekea kuongezeka kwa shinikizo la damu.Hii inaweza kufanya mishipa midogo ya damu(blood carpillary) ilioko kwenye ubongo kupasuka na kupelekea kifo.




3.Matumizi ya pombe kupita kiasi. Pombe huathiri mfumo wa neva unoongoza utendaji kazi wa moyo kwa kuongeza mapigo ya moyo ( sympathetic activity ) na kupekea moyo kusukuma damu kwa nguvu na kupelekea kuongezeka kwa shinikizo la damu.


4.Matumizi ya chumvi kupita kiasi. Chumvi inapokuwa nyingi kwenye damu husababisha kusharabiwa kwa maji mengi kuingia kwenye damu na kuongeza ujazo wa damu mwilini .Hali hii hufanya kuongezeka kwa shinikizo la damu .

5.Matatizo ya figo kushindwa kufanya kazi( Renal failure). Figo inaposhindwa kufanya kazi husababisha kushindwa kuchuja damu ipasavyo.Hali hii husabisha maji mengi kubaki mwilini na kusababisha kuongezeka kwa shinikizo la damu.



DALILI ZA MTU KUWA NA SHINIKIZO KUBWA LA DAMU

Shinikizo la damu katika hatua za mwanzoni halina dalili zinazoweza kuonekana dhahiri.(asymptomatic) .Hili ni tatizo linalowapata watu wengi bila ya mtu kuona mabadiliko yoyote ambapo pressure huongezeka siku baada ya siku hatimaye kufikia katika hatua ya juu na kusababisha kifo.Katika hatua ambapo shinikizo la damu kuwa kubwa hugundulika dalili zifuatazo huambatana na mgonjwa.

  1. Maumivu ya kichwa.















    2.Kutokwa na damu puani kutokana na kuongezeka kwa pressure ya damu .









                                                                                                                                                                                                                                             
3.Maumivu ya kifua







4.Kuwa na matatizo ya macho .Hii inatokana na na kuharibiwa kwa mishipa ya damu midogo inayopeleka damu kwenye retina ya jicho inayosaidia macho kuona na hatimaye kusababisha kushindwa kuona vizuri (Hypertensive retinopathy).

5.Kuwa na uchovu na kubadilika kwa kasi ya mapigo ya moyo.


NJIA ZA KUEPUKA KUPATA SHINIKIZO KUBWA LA DAMU


  1. Fanya mazoezi ya viungo vya mwili . Njia hii hufanya mwili kuweza kuyeyusha mafuta ya ziada yaliyo kwenye mishipa ya damu na ogani nyingine mwilini ili kutoa nishati. Mazoezi pia hufanya mzunguko wa damu kuwa mzuri na kuleta afya bora.








   2. Epuka kula vyakula vyenye mafuta mengi hasa mafuta ya wanyama.(cholesterol free).Mfano kula vyakula vyenye mafuta kiasi  pamoja na kuhakikisha uwiano wa vyakula vya aina zote katika mlo kamili uko sahihi. Hii itasaidia kupunguza kuongezeka kwa kiwango cha cholesterol kwenye damu na kukuepusha kupata shinikizo la damu.



3.Epuka kunywa pombe kupita kiasi. Tabia hii itasaidia kupunguza uwezekano wa kupata shinikizo la damu kutokana na matumizi ya pombe kupitiliza .Kilevi huambatana na madhara ya muda mfupi na ya kudumu kwa afya zetu hivyo epuka pombe kupita kiasi.




4.Tumia kiasi kidogo cha chumvi kwenye chakula.

5.Punguza mambo yanayoweza kukuletea msongo wa mawazo. Hakikisha mwili wako unajishughulisha pamoja na kukaa pamoja na marafiki au vikundi vinavyojenga mawazo chanya.


LINKS

1.http://emedicine.medscape.com/article/241381-overview#a7

2.http://www.webmd.com/hypertension-high-blood-pressure/guide/hypertension-symptoms-high-blood-pressure

3.http://www.mayoclinic.org/diseases-conditions/high-blood-pressure/in-depth/high-blood-pressure/art-20046974

Prepared by Andrew Luhusa MD  Student @ MUHAS

           30th sept 2016


Friday, September 23, 2016

HOMA YA MAPAFU( PNEUMONIA)

    HOMA YA MAPAFU (PNEUMONIA)

  Pneumonia ni ugonjwa wa mfumo wa upumuaji unaoambatana na kupungua ufanisi wa  mbadilishano wa gesi kati ya binadamu na mazingira yake ya nje (atmosphere). Hali hutokana na maambukizi kwenye njia ya  hewa yanayosababishwa na bacteria au virusi. Mfano wa bacteria wanaoweza kuleta maambukizi ya homa ya mapafu ni aina ya Streptococcus pneuomoniae  wakati aina ya virusi kama influenza virus na  Respiratory syncytial virus(RSV)  husababisha maambukizi kwenye njia ya hewa na kupelekea homa ya mapafu. Pneumonia huenezwa kwa njia ya hewa ama kugusana  na mgonjwa
     
          Ugonjwa huu huwapata hasa watoto na wazee  kutokana na  kutokuwa na mfumo imara wa kinga ya mwili .  Watu wenye matatizo katika mfumo wa upumuaji kama vile pumu(asthma) wakipata maambukizi hali yao huzidi kuwa mbaya zaidi.


DALILI ZA MTU MWENYE PNEUMONIA

Maambukizi mara nyingi husababishwa na bacteria ambao husababisha dalili zifuatazo
1.Kikohozi kinachoambatana na makohozi mazito ambayo yaweza kuwa na rangi ya kijani au kuambatana na damu.

2.Kuwa na homa .Homa husababishwa na bacteria kutoa kemikali (pyrogens) ambazo huingilia mfumo wa kawaida wa urekebishaji jotoridi la mwili na kufanya mwili kuongeza joto lake ili kuweza kuzuia au kuua vimelea mwilini.  Kadiri bacteria walivyowengi mwilini ndivyo jotorid hongezeka na kupelekea homa kali ya mapafu.

3.Kupumua harakaharaka na pumzi fupi.. Hali hii hutokea kutokana mwili kupungukiwa gesi ya oxygen kutokana na kupungua ufanisi wa utendaji kazi wa njia ya hewa kunakosababishwa na maambukizi ya bacteria; hivyo kuulazimu mwili kutumia nguvu ya ziada kwa kuongeza kasi ya upumuaji.

4..Maumivu ya kifua .Hali hii hutokea wakati wa kuvuta pumzi ndani au kipindi mgonjwa anapokohoa

 5.Kuongezeka kasi ya mapigo ya moyo.Moyo huongeza kasi ya mapigo yake illi kuhakikisha kuwa mwili mzima unapata oxygen kutokana na kupungua ufanisi wa upatikanaji wa oxygen kwa mfumo wa kawaida wa hewa.



ATHARI ZA PNEUMONIA KWENYE MWILI WA BINADAMU

Pneumonia husababisha mwili kushindwa kupata oxygen ya kutosha hivyo kusababisha athari mbalimbali zinazotokana na mwili kupungukiwa oxygen .Mfano wa athari hizo ni kama hypoxemia ambapo kiwango cha oxygen kwenye damu hupungua na kupelekea tishu kushindwa kupata oxygen ya kutosha kwa ajili ya kuzalisha nishati ya mwili.(hypoxia).
        Cyanosis ni tatizo linaloweza kujitokeza ambapo damu ambayo haina oxygen inapokuwa kwa wingi mwilini kuliko yenye oxygen hasa kwa watoto na kumfanya mtoto aonekane kuwa na rangi ya blue .  .Hypercabia na hypercapnea  ni hali inayotokea ambapo kiwango cha carbondioxide kwenye damu na kwenye tishu huongezeka. Kama maambukizi hayakutibiwa yaweza kusababisha kifo.

NJIA ZA KUJIKINGA NA PNEUMONIA

  1. Weka mazingira katika hali ya usafi. Hii inapunguza uwezekano wa kuchukua vimelea kutoka sehemu mbalimabli endapo mgojwa wa pneumonia aliyegusa vifaa ambavyo mtu mwingine atatuma
  2. Usitumie sigara kwani moshi wa sigara hupunguza uwezo wa mapafu kudhibiti vimelea vya pneumonia na hivyo kufanya kuwepo uwezekano wa  kuambukizwa pneumonia
      3.Chanjo ya pneumonia pia hutolewa ili kujikinga na ugonjwa huu.

2.http://www.m.webmd.com/a-to-z-guides/tc/pneumonia-topic-overview

Prepared by Andrew Luhusa MD Student @ MUHAS

                           23 Sept 2016

Friday, September 16, 2016

TYPHOID & KIPINDUPINDU

                             TYPHOID   NA  KIPINDUPINDU


Magonjwa haya mawili ni miongoni mwa magonjwa yaliyo katika kundi la magonjwa yaenezwayo kwa njia ya maji na chakula . Pia huambukizwa na vimelea vya aina tofauti ya bacteria .Ni magonjwa hatari endapo hayakupatiwa tiba sahihi mapema.


            TYPHOID

Typhoid fever ni ugonjwa hatari unaosababishwa na vimelea aina ya bacteria viitwavyo Salmonella typhi ;ambavyo hushambulia mwili kwa kutoa sumu ambazo huleta dalili mbalimbali kwenye miili yetu..



           DALILI ZA MTU MWENYE TYPHOID

  1.  Maumivu ya tumbo kwa mda mrefu
  2. Kushindwa kupaata choo kwa urahisi ( constipation)
  3. Kupanda kwa jotoridi  mwili na  homa (karibu 39' C au 103 F)
  4. Kupatwa na vidonda vidogo  vyekundu(rose spots)
  5. kupata matatizo ya akili endapo typhoid haikutibiwa mapema
   
.
                                      NJIA ZA KUENEA KWA TYPHOID

                 
  1. Typhoid huenea kwa njia ya maji na chakula kama  havikuandaliwa kuwa salama kwa matumizi ya binadamu. Maji machafu ni mazingira mazuri kwa ukuaji wa bacteria wa ugonjwa huu .Maji machafu kutoka chooni au mtaroni yaweza kuwa na vimelea ambavyo vimetoka kwa mtu ambaye ni mgonjwa au ambaye ametibiwa lakini vimelea vikabaki mwilini mwake (carrier). Pindi maji haya yanapochanganyika na maji safi na salama au kutumika kupika chakula ambachohakikuchemka vizuri huingia katika miili yetu.
     
2.Uandaaji vyakula unaweza kuwa moja ya njia ya kuenea kwa typhoid. Mtu mwenye maambukizi ya ugonjwa huu anaweza kuacha vimelea kwenye matunda na vyakula . Vyakula na matunda yaliyotayarishwa kwa njia hii huwa na uwezekano mkubwa wa kueneza typhoid.


                       NJIA ZA KUJIKINGA (KUZUIA)  NA TYPHOID

  1. Osha matunda vizuri kabla ya kula.Tabia hii pamoja na kuosha viungo kama nyanya,mboga za majani na pilipili hoho kabla ya kuvipika. , itasaidia kuondoa vimelea ama kuvipunguza kabla ya kupika, hivyo kupunguza athari zinazoweza kujitokeza ikilinganishwa na kutozingatia usafi wa vitu hivi.

2. Nawa mikono kwa maji na sabuni kabla ya kula chakula,.Kunawa mikono kwa sabuni (medicated soap) kunaweza kuondoa vimelea ambavyo vingeweza kusababisha magonjwa kwa kuwa sabuni huua vijidudu vya magonjwa.







    
   3. Tumia  maji ya kunywa yaliyo  safi na salama . Maji ya kunywa yanaweza kuwa salama endapo yatachemshwa vizuri na kuhifadhiwa katika mazingira masafi ama kwa kuyatibu  kwa kutumia  dawa kama vile water guard. Jenga mazoea ya kunywa maji safi kila mahali unapokuwa kuepusha hatari ya kupata typhoid.


4.Chanjo ya typhoid hutolewa   na baadhi ya nchi duniani kama vile Uingereza ili kupunguza kasi ya ueneaji wa typhoid. Njia hii bado haijaanza kutumika na nchi nyingi duniani hasa  zile zinazoendelea .Endapo njia hii ikifanikiwa kutumika nchini kwetu tutaweza kupunguza kasi ya maambukizi na ueneaji wa typhoid.



                                      KIPINDUPINDU 

Vibrio cholerae
Kipindupindu ni ugonjwa unaosababishwa na bacteria aina ya vibrio cholerae ambao hushambulia mfumo wa chakula hasa kwenye utumbo  kwa kutoa sumu iitwayo enterotoxin ;ambayo husababisha maji mengi kutoka mwilini na kujaa kwenye utumbo (intestinal lumen) na kupunguza uwezo wa kusharabiwa kwa maji kuingia kwenye mfumo wa mzunguko wa damu. Hali hii hupelekea  kuharisha sana na kupoteza maji mengi mwilini.


  DALILI ZA KIPINDUPINDU

  1. Kuongezeka kwa mapigo ya moyo
  2. Kushuka kwa shinikizo la damu
  3. Ngozi ya mwili kukakamaa na kupoteza uwezo wa kuvutika (elasticity)
  4. Kukauka mdomo na macho 
  5. Kusikia kiu ya kunywa maji na kubanwa misuli(Muscle cramp)

Dalili hizi hutokea kutokana na kupotea kwa maji  na ions kwenye mwili kutokana na kuharisha mfululizo kwa muda mrefu.
 
NJIA ZA KUENEA KWA  KIPINDUPINDU  

  1. Kipindupindu huenezwa hasa kupitia chakula na maji yaliyo na vimelea vya ugonjwa. Kwenye maeneo ambayo usafi hauzingatiwi ni miongoni mwa maeneo yaliyo kwenye hatari na kukumbwa na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu.Mfano katika makazi ya wakimbizi ni rahisi kuchaganyika vyanzo maji safi na machafu.


2.Kutokutumia choo kwa ajili ya kujisaidia  na kujisaidia ovyo,huweza kusababisha bacteria kutoka kwa mgonjwa wa kipindupindu na kuingia kwenye vyanzo vya maji safi. Pindi mtu atakapotumia maji yaliyo na vimelea vya ugonjwa, atapata kipindupindu .









3.Kula matunda pasipo kuyaosha ni hatari kwa afya zetu kwani yaweza kuwa na vimelea vya kipindupindu. Mtu atakapokula matunda huingiza na bacteria mwilini mwake ambao huweza kuleta ugonjwa huu ama magonjwa mengine kama typhoid.











             NJIA ZA KUJIKINGA NA KIPINDUPINDU

  1. Tumia maji safi na salama
  2. Tumia choo kwa haja kubwa na ndogo
  3. Osha matunda kabla ya kula
  4. Epuka kula vitu maeneo yenye msongamano wa watu 
LINKS:
http://www.webmd.com/a-to-z-guides/cholera-faq#1

http://emedicine.medscape.com/article/231135-medication

http://cdn.phys.org/newman/gfx/news/hires/cholerastalk.jpg


Prepared by Andrew Luhusa ;MD Student at  Muhimbili University of Health and Allied Sciences(MUHAS)
                                              15  Sept 2016

Friday, September 9, 2016

BINADAMU , MAZINGIRA NA MAGONJWA

  UHUSIANO      KATI   YA BINADAMU,              MAZINGIRA        NA      MAGONJWA

BINADAMU
Miongoni mwa viumbe hai wanaoishi duniani binadamu ni kiumbe anaechukuliwa kuwa na utashi wakuelewa mambo mbalimbali .Katika jamii yetu kila  mwanadamu amezungukwa na vitu mbalimbali ambavyo kwa ujumla wake hufanya mazingi
ra yake anayoishi.Mfano ,watu,hewa,maji na mimea hufanya maisha ya binadamu kuwa endelevu duniani.

MAZINGIRA
Jumla ya vitu vyote vinavyomzunguka mwanadamu hufanya mazingira yake yakuishi.Wanadamu tumezungukwa na na vitu mbalimbali kama vile hewa yenye gesi mbalimbali,vyanzo vya maji,ardhi pamoja na viumbe wengine wanaonekana na wasioonekana kama bacteria na virusi.


Moshi kutoka  viwandani  huchafua mazingira.






MAGONJWA
Ugonjwa ni hali ya kuwa  na afya dhaifu kutokana na kushambuliwa na vimelea vya magonjwa(pathogens) ,ukosefu wa virutubisho,sababu za urithi(genetic) na magonjwa yatokanayo na mazingira(environmental factors) .hali hii hudumaza kinga ya mwili na kupelekea hali mbaya kiafya.
       


                           ATHARI YA MAZINGIRA KWA AFYA YA BINADAMU

Hewa, maji ,chakula na mimea na vimelea kama mfano wa vitu vinavyomzgunguka mwanadamu ,vina athari kwa afya ya binadamu upale vinapochafuliwa ama kumwingia binadamu moja kwa moja(mfano,bacteria,virus na fungus).Kuchafuliwa kwa hewa kutokana na moshi wa viwanda(carbondioxide) na gesi nyingine kama sulphurdioxide huweza kusababisha magonjwa ya mfumo wa upumuaji kama vile pumu na kuongeza hatari ya kupata kifua kikuu(tuberculosis).
         Uchafuzi wa vyanzo vya maji kutokana na kemikali na kuingiliana kwa mfumo wa maji taka na maji safi ni sababu inayopeleukea magonjwa ya mlipuko  kama kipindupindu,na kuhara pamoja na typhoid. Vyakula ambavyo havikuhidhawia vizuri na ukosefu wa lishe bora ni moja ya sababu zinazopelekea baadhi ya magonjwa kama tumbo la kuharisha(dysentery),na kwashiorkor. Mazingira machafu ni makazi ya vimelea vya magonjwa kama vile bacteria na fungus .vimelelea hivi huingia ndani ya mwili na kuushambulia na hatimaye kuzorota kwa afya.
                     
                     


NJIA ZA KPUNGUZA/KUONDOA  ATHARI ZA MAZINGIRA KWA AFYA YA BINADAMU
Baada ya kuona sababu mbalimbali zinazoathiri afya ya binadamu tuangalie nini kifanyike ili kuondokana na athari zinazotokana na uhusiano kati ya mazingira yetu na afya zetu .(1)Kwanza kabisa tutambue mazingira yetu vema ili kujua namna ya kuyadhibiti,kwa mfano uwepo wa viwanda vinavyotiririsha kemikali kwenye vyanzo vya maji  karibu na maeneo yetu ya kuishi. (2)Kujenga mazoea ya kufuata kanuni za afya kutatuwezesha kuepukana na magojwa mengi , kwa mfano matumizi ya choo,kuosha matunda kabla ya kula,,kula nyama iliyoiva vizuri kuhakisha hakuna vimelea vinavyowezakuishi pamoja na kutumia maji safi na salama.(3)Kuzingatia lishe bora ni njia inayoweza kuondoa athari ambazo zingesababishwa na lishe duni kama kwashiokor kwa watoto chini ya miaka mitano,upungufu wa damu(pernicious anaemia) na magonjwa ya macho.(4)Kujifunza zaidi elimu ya afya  miili yetu ili kuongeza ufahamu juu maswala mbalimbali ya kiafya,kwa mfano kupitia mtandao kwenye blogs kama hii na semina mbalimbali za afya ya jamii.(5)Kushiriki katika  mipango mbalimbli ya afya kama vile chanjo kutakuwezesha kujikinga na magonjwa ambayo yaweza kusababisha kuzorota kwa afya yako.
              Kwa ujumla afya yako ni muhimu sana kwa ajili ya kukufanya ushiriki katika shughuli mbalimbali za kila siku.Hivyo ni tunawajibu wa kutunza afya zetu kwa ajili ya maendeleo yetu.
 Endelea kufuatialia mada ijayo uzidi kujifunza afya yako ili kukusaidia wewe na mtu mwingine.

                                               
                                     JINSI TUNAVYOPATA MAGONJWA    KUTOKA  
                                                    KWENYE MAZINGIRA YETU

REFERENCES
435,d.d24tp://scholar.google.com/scholar?q=environmental+pollution+and+tuberculosis&hl=en&as_sdt=0&as_vis=1&oi=scholart&sa=X&ved=0ahUKEwjy4I_bs4LPA

https://www.google.com/url?sa=t&rct=j&q=&esrc=s&source=web&cd=1&cad=rja&uact=8&ved=0ahUKEwil3-XXtoLPAhUBJcAKHVJbCskQFggfMAA&url=http%3A%2F%2Fwww.tanzaniatoday.co.tz%2Fnews%2Fwizara-ya-afya-yatoa-semina-kwa-wanahabari-dar&usg=AFQjCNGKIPuYA97V2VTGXnGf5HeF8jHu5A&sig2=nmU0IoGNjc_10ZoF3AYy_Q

http://www.ncbi.nlm.nih.gov/pubmed/20083235#

Saturday, September 3, 2016

WELCOME IN MY BLOG

                   WELCOME  LADIES AND GENTLEMEN                               
IN MY HEALTH INFO SHARE BLOG  TO LEARN AND GET APPLICABLE RESULTS                         IN YOUR HEALTH.
THANK YOU